| ENG Swahili SPA Swahili |
.e
asili
Kiswahili ni lugha ya Kibantu iliyoanzia katika pwani ya Afrika ya Mashariki takribani karne ya tisa (Nurse na Spear 1985: 49). Kikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, Kiswahili ni lugha rasmi ya Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda, na pia ni mojawapo ya lugha nne za kitaifa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha, huzungumzwa kwa mapana katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki, yakiwemo Burundi, kaskazini mwa Msumbiji, Somalia na Visiwa vya Komoro.
Tangu karne ya kwanza BK, pwani ya Afrika ya Mashariki imeshirikiana katika biashara ya Bahari ya Hindi, hali iliyochangia kuibuka kwa eneo lenye lugha mbalimbali, uhamaji wa watu, na mahusiano ya aina mbalimbali ya kimataifa na ya kuvuka mabara (Pearson 2003: 78). Kiswahili kina historia ndefu ya kifasihi inayorejea angalau karne ya kumi na sita, wakati ambapo utamaduni wa maandishi kwa kutumia hati ya Kiarabu ulipokua na kuanza kustawi. Utamaduni huu ulijikita sana katika ushairi ulioandikwa na ulamaa—yaani wanazuoni na makadhi wa Kiislamu.
Katika historia yake ya karne nyingi, fasihi ya Kiswahili imekuwa ikipokea maandishi yaliyosambaa kupitia biashara, uhamiaji, mabadiliko ya kisiasa, mapambano ya utawala na ukombozi, pamoja na ushirikiano wa kimataifa. Katika kipindi cha sasa, uwanja wa fasihi ya Kiswahili unaendelea kuwa hai na wa kusisimua, ukichochewa na tuzo za fasihi kama vile Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, utamaduni wa mashairi ya magazetini unaozidi kushamiri, na pia kuongezeka kwa majukwaa ya mtandaoni yanayochapisha kazi maarufu za Kiswahili.
.
ikisiri
Makala hii inatoa historia fupi ya tafsiri kutoka na katika Kiswahili, mojawapo ya lugha kuu za Kibantu inayosambaa katika eneo la Afrika ya Mashariki, kwa kuzingatia hasa maandishi ya kifasihi.
Sehemu inayohusu tafsiri katika Kiswahili imepangwa kwa kuzingatia vipindi muhimu vya kihistoria. Kipindi cha kwanza kinahusu kabla ya karne ya ishirini, wakati ambapo pwani ya Kiswahili, ilikuwa imeunganishwa na njia za biashara za Bahari ya Hindi pamoja na mitandao ya kielimu ya Kiislamu, hali iliyofanya pwani hiyo iwe kitovu cha lugha nyingi na utamaduni mbalimbali. Katika muktadha huo, tafsiri ilichukua nafasi kubwa. Kipindi cha pili kinachunguza kazi ya wamisionari na matumizi ya tafsiri chini ya tawala za kikoloni za Kijerumani na baadaye Kiingereza. Kipindi cha tatu kinahusu miaka ya 1960, wakati ambapo tafsiri iliingiliana na harakati za uhuru, ajenda za ujenzi wa taifa, pamoja na miungano ya kitamaduni na kisiasa. Kipindi cha nne kinachambua maendeleo tangu miaka ya 1990, kipindi kilichoshuhudia kuongezeka kwa hamasa mpya katika tafsiri ya kifasihi katika Kiswahili, hali iliyohimizwa na mikakati ya kitaaluma, asasi za paradiplomasia, na soko la uchapishaji lililozidi kuwa na mseto.
Sehemu inayohusu tafsiri kutoka Kiswahili imegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inazingatia tafsiri zilizofanywa na wamisionari pamoja na wasomi, waliotoa mchango mkubwa katika kuandika na kuhifadhi utajiri wa fasihi ya Kiswahili. Sehemu ya pili inahusu maendeleo tangu miaka ya 1970 na baadaye, ikionyesha jinsi Kiswahili kilivyozidi kuwa lugha chanzi ya tafsiri, huku pia ikibainisha mipaka ya miradi hiyo, ambayo mara nyingi imejikita zaidi katika nyanja ya kitaaluma.
Sehemu nyingine za makala hii zinajikita katika uimarishaji wa kitaasisi wa taaluma ya tafsiri kama fani katika miktadha ya jamii zinazozungumza Kiswahili. Tangu mwishoni mwa miaka ya 1980, uwanja huu umetambuliwa rasmi katika ngazi za kitaaluma na kitaasisi, hasa nchini Kenya na Tanzania. Upanuzi huo unaakisiwa na kuanzishwa kwa programu za vyuo vikuu, kuandaliwa kwa makongamano yanayolenga tafsiri, kuundwa kwa vituo maalumu na vyama vya kitaaluma vya wafasiri na wakalimani, pamoja na kuongezeka kwa maandishi ya kitaaluma yanayochunguza tafsiri katika na kutoka Kiswahili. Makala inahitimisha kwa kubainisha maeneo muhimu yanayohitaji utafiti zaidi katika siku zijazo.
record
| Serena Talento | |
| 2026 | |
| Talento, Serena. 2026. "Kiswahili" @ ENTI (Encyclopaedia of Translation & Interpreting). AIETI. | |
| https://doi.org/PENDING | |
| https://www.aieti.eu/enti/swahili_SWA |